JINSI YA KUANDAA HYDROPONICS FODDER KWA AJILI YA MIFUGO YAKO
Leo tunazidi kukuwezesha kutambua fursa lukuki ambazo zinazoweza
kufanywa na yeyote katika jamii yetu.Leo tutaangalia juu ya
hydroponic. Katika kuangalia tutagusia vipengele vifuatavyo:
• Utangulizi,
• Faida ya matumizi ya hydroponic,
• Jinsi ya kuandaa,
• Umwagiliaji,
• Uvunaji,
• Mfano halisi,
• Upatikanaji wa chakula kwa muda wote,
• Hitimisho.
UTANGULIZI
HYDROPONIC ni sayansi/sanaa ya kuotesha mazao bora yenye tija kwa muda
mfupi zaidi bila kutumia udongo kabisa, kwa kutumia maji na virutubisho
(Hydroponic Nutrients).
HYDROPONIC HYDROPONICS FODDER – ni kimea kinachooteshwa kwa kutumia
mbegu za shayiri au ngano ili kupata chakula cha mifugo mfano kuku,
ng’ombe, sungura, nguruwe, mbuzi, kondoo n.k
Ili kuotesha mbegu zako kwa utaratibu huu utahitaji kuwa na banda maalum
kwa kuoteshea lenye ukubwa wowote, trei za plastic au aluminium zenye
matundu (kama ni aluminium hakikisha sio material yale yanayopata kutu
pindi yakiingia maji).
Pia utahitaji kuwa na virutubisho vya hydroponics (Hydroponics
Nutrients), Sprayer (Chupa ya kunyunyiza maji yenye matundu madogo ili
maji yamwagike kama mvua), Mbegu za shayiri au ngano (chagua mbegu
ambazo hazijashambuliwa na wadudu), na pia unatakiwa uwe na chombo cha
kuloweka mbegu na hapa waweza kutumia ndoo ya aina yoyote, kwani
itatakiwa uziloweke kwa siku chache.
Sayansi hii ya uoteshaji wa mbegu mbalimbali madhumuni makubwa sana ni
kwaajili ya mifugo kama vile, Kuku, Mbuzi, Ng’ombe, kondoo na kazalika,
ila kama ni mboga inaweza itwa hydrponic tomatoes na kazalika kulingana
na aina ya mbegu husika.
FAIDA YA MATUMIZI YA HYDROPONIC
Ili kuweza kukupatia picha halisi tunakufahamisha kwanza faida zilizopo
za matumizi ya hydroponic fodder kwa mifugo.Kwa uchache baadhi ya faida
hizo ni:
• Ni nafuu sana kulinganisha na garama za CHAKULA cha madukani au viwandani.
• Kina virutubisho na vitamini mara 3 zaidi ya CHAKULA cha kawaida cha Mifugo.
• Hupunguza magonjwa ya mfumo wa hewa kama vile mafua kwa mfugaji na Mifugo kwani hakina vumbi kabisa.
• Kina protein na Energy/nishati nyingi zaidi mara 3 ya inayopatikana kwenye vyakula vya kawaida vya Mifugo kama kuku.
• Mifugo hukua haraka sana kutokana na wingi wa protein ambayo hufanya Kazi ya kujenga mwili na kukuza.
• Chakula hiki ni laini sana na kitamu kwa kuku na mifugo yote (palatable).
• Mmeng’enyo wa chakula hiki huongezeka kutoka 30% kwa chakula cha
kawaida hadi 95% kwa chakula cha hydroponiki hivyo chakula kingi
kutumiwa na mwili wa mifugo na kupunguza kinyesi na usumbufu wa
usafishaji wa banda.
• Kinyesi hupungua na kuwa kati ya 5%-10% tu kwani chakula kingi humeng’enywa na kutumiwa na mwili wa mifugo.
• Mazao kama mayai au maziwa huongezeka kwa 40% kulinganisha na chakula cha kawaida.
• Kiini cha yai la kuku anayelishwa hydroponic fodder huwa cha njano sana hata kama ni kuku wa kisasa.
• Hupunguza garama za ufugaji kwenye manunuzi ya chakula kwa 50-75% hivyo kuongeza faida.
Pamoja na mnyumbulisho wa baadhi za faida ya matumizi ya teknolojia hii
hapo juu,kiujumla ni rahisi kutumia teknolojia hii kwani inaweza
kufanyika mahali popote. Husaidia kuvuna na kupata mazao mengi kwa muda
mfupi. Haina madhara kwa afya za mifugo na binadamu kama mlimaji
alizingatia maelekezo.
JINSI YA KUANDAA
Tumefanya tafiti kufahamu hatua kadhaa zinazopitiwa ili kufanikisha
zoezi la upandaji.Zifuatazo ni baadhi ya hatua ambazo tumefanikiwa
kukutana nazo:
• Chukua mbegu zako kisha zisafishe vizuri kuondoa takataka zote.
• Weka maji kwenye ndoo safi na kisha weka mbegu zako ili kuziloweka
kwa muda wa masaa 4 au zaidi ukipenda masaa 12.Muda mrefu zaidi
huwezesha mbegu kuchipua vizuri na kwa haraka.
• Baada ya masaa 4 au 12 kupita toa mbegu zako kwenye ndoo na uzichuje maji kwa kutumia chujio au kitambaa kisafi.
• Baada ya kuchuja maji hamishia mbegu zako kwenye tray kisha
zisambaze ili zisibanane kupita kiasi. Kwa kuanzia fursa hii unaweza
kutumia tray yeyote hata ungo unafaa kwa kuanzia .
• Baada ya kuweka mbegu zako kwenye tray funika tray yako kwa muda wa
masaa 48 (SIKU 2) tumia mfuniko wenye matundu madogo madogo na
machache.
• Baada ya masaa 48 kupita (siku 2) mbegu zako zitakuwa zimechipua kikamilifu, utaona mfano wa nyuzi nyeupe zinachomozo.
• Hamishia tray zako kwenye kichanja au eneo lenye hewa ya kutosha
lakini zikinge dhidi ya jua kali kwa kuweka turubai au nailoni juu ya
kichanja unaweza pia kutumia hata mifuko ya unga (viloba) kutengeneza
kichanja, unaweza pia kuzungusha wavu kama net za mbu ili kuzuia wadudu
i.e inzi na pia kama eneo lako lina ndege wengi basi kutumia net itakuwa
msaada kwako ili kuwazuia ndege hao.
UMWAGILIAJI
Mwagilia angalau mara 3 kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni. Hakuna
haja ya kumwagilia usiku kwa sababu hewa ya usiku huwa imepoa na kubeba
unyevu wa kutosha na hata asubuhi usishangae kukuta umande kwenye
fodder yako.
UVUNAJI
Unaweza kuvuna fodder yako ndani ya siku 7 au 9.Ingawa wapo wengi
wanavuna haraka yamkini ili kukidhi uhitaji kwa wakati husika.Lakini
makala nyingi zinaelekeza siku 7 au 9.
MFANO HALISI
Kawaida teknolojia hii kwa mfano ukitumia kilo moja ya mbegu za ngano
unaweza kupata mpaka kilo 8 za chakula cha kuku.Kwahiyo kwa wafugaji wa
kuku na mifugo mingine hii ni fursa nzuri ya kupunguza gharama za
malisho ya mifugo hii.
Ni vyema kufahamu kuwa katika kilo moja ya ngano utakuwa umeokoa
manunuzi mengine ya kilo saba kwa kutumia teknolojia hii basi jamii
ikitambua fursa hii itawasaidia sana katika malisho ya mifugo yao.
UPATIKANAJI WA CHAKULA KWA MUDA WOTE
Ili uweze kuhakikisha chakula cha njia hii kinakuwa tayari kwa malisho
ya kuku wako kila siku lazima ujue mahitaji halisi ya chakula kwa siku
moja.
Kwa mfano kama kuku wako wanatumia kilo 50 kwa siku. Kutokana na matokeo
ya tafiti kwamba kilo 1 za mbegu zinazalisha kilo 8 za fodder kwa siku
8, je unahitaji mbegu kiasi gani kutengeneza fodder ya kuwatosha kuku
wako wote 350 kwa siku?.Sasa kilo 50 gawanya kwa kilo 8 za fodder
uliyoipata kutokana na kilo 1 za mbegu, jibu lake litakuwa ni 6.25 .Hizi
kilo 6.25 ni sawa na kilo za mbegu nitakazotakiwa kuotesha kila siku
ili kukidhi haja ya ufugaji wako.
Kwa maana hiyo itakulazimu kupanda kilo 6.25 za mbegu kila siku katika
tray kubwa zenye uwezo wa kubeba kilo 6.25 za mbegu. Kama utatumia tray
moja kubwa kupanda mbegu zote hizo itakulazimu uwe na tray 8 za namna
hiyo kwa sababu utakuwa unapanda mbegu kwenye tray kwa kupishanisha siku
moja moja kwa maisha yote ya ufugaji na kila tray inapovunwa
inasafishwa na kupandwa mbegu zingine siku hiyo hiyo.
HITIMISHO
Wataalamu wengi wanashauri kuwa iwapo utaamua kutumia njia hii kama
chakula cha kuku ni vizuri pia kuwapa kuku punje kavu au mapumba matupu
kwa uwiano wa 2 kwa 10 ili kuhakikishwa kwamba mmengenyo wa chakula
unafanyika vizuri pasipo kuleta hatari ya constipation na siyo lazima
kufanya hivyo kila siku. Virutubisho vilivyo kwenye fodder ya ngano au
fodder ya shairi ni vya kutosha kabisa kwa mahitaji ya kuku wako.
Lakini tunakiri kuwa fursa hii sio kwa wafugaji tu,bali wajasiriamali
wanaweza kuiangalia fursa hii kwa mapana zaidi ili kuona namna gani
wanaweza kuwekeza na kuanza kuuza kwa wafugaji wa fursa hii.
Ni fursa ambayo imeanza kufatiliwa kwa wingi kwa sasa.Nasi tunaimani
makala hii itakuwa imekupa mwanga zaidi kwa ajili ya kuifatilia kwa
mapana fursa hii.
Tunazidi kuwashauri kuzidi kufatilia zaidi fursa hii kwa wataalamu wa
kilimo wa serikali na taasisi au makampuni ya kilimo yanayotambulika ili
kuweza kupata ushauri zaidi kwa ajili ya kilimo chenye tija kwa mipango
midogo na mikubwa.
Imeandaliwa na Edlork Team,
Enter your comment...nawezaje kupata hydroponics nutrients mimi niko dar es salaam, kimara
ReplyDeleteAhsante sana kwa somo,hiyo Hydroponics nutrints upatikanaji wake ukoje maana uliyopo mikoani ni shida
ReplyDelete