MAHITAJI
1. Kuku(tetea) 10 na Jogoo 01
2. Banda bora
3. Vyombo vya chakula na maji
4. Chakula bora
5. Madawa na chanjo kwajili ya magonjwa
6. Chanzo cha nishati joto na mwanga
7. Elimu na ujuzi wa malezi bora
8. Chombo au chumba cha kutunzia vifaranga
9. Mayai ya kuku wa kisasa/mayai mabovu(ambayo hayakuanguliwa)
10. Madaftari au kitabu cha kutunzia kumbukumbu
KUKU (MATETEA) 10
Wakati wa kuanza mradi wako hakikisha una kuku 10 (matetea) wenye umri sawa na hawajawai kutaga hata mara moja. Chagua kuku wenye rangi nzuri kutoka katika familia bora kutegemea malengo ya mradi wako. Mfano kama lengo lako ni kuzalisha kuku wa kienyeji kwajili ya nyama basi chagua mbegu ambayo inakuwa haraka na yenye uzito mkubwa. Au ikiwa lengo ni mayai basi ni vema kuchagua aina ya kuku yenye kukua haraka na kutaga mayai mengi.
Ili kupunguza gharama za manunuzi ya kuku na hivyo kuongeza faida kwa mfugaji ni vema kununua kuku wadogo ambao wametoka tu kuachishwa kulelewa na mama zao. Kuku hawa utawapata kwa bei ya chini, tena watafaa sana maana watakua na umri mmoja pia.
JOGOO 01
Jogoo mmoja tu anatosha kuwahudumia kuku matetea yote kumi. Hakikisha katika uchaguzi wa jogoo bora lililochangamka, rangi nzuri, upanga umesimama, macho angavu, uzito wa kutosha, na uwezo mkubwa wa kuzalisha. Ni vema mfugaji akaelewa kwamba kuku wote watakaozalishwa watategemea ubora wa jogoo wake. Uwezo wa kutaga kwa kuku na upatikanaji wa mayai pia hutegemea kwa karibu ubora wa jogoo aliyechaguliwa.
JINSI YA KUFANYA
Wakuze kuku wako hadi watakapofikia muda wa kutaga. Wakianza kutetea ni kiashiria kwamba wakati wa kutaga umekaribia hivyo andaa viota kwajili ya kutagia.
Viota vinapaswa viwe na ukubwa stahiki ili kumwezesha kuku kuyafunika mayai yote vizuri wakati wa kuetamia, viota viwe vinavyozuia mayai kutawanyika, viwe mahali pakavu na safi.
Hakikisha kuku wote wanataga katika viota tofauti. Kuku anapotaga mayai matatu unapashwa kuchukua mayai mawili na kumwachia yai moja ili kumfanya aendelee kutaga zaidi. Kuku akifikia yai la kumi na mbili anza kumwachia mayai matatu ili kumwandaa kwa kazi ya kuetamia. Kwa kufanya hivi, kuku atataga mayai 15 au zaidi na ikiwa atataga mayai 15 au chini ya hapo nakushauri utafute mayai mengine ujazilizie ili kufikisha mayai 20 kwa kila kuku. Zingatia kwamba mayai unayoyatoa kwa kila kuku, yanatunzwa sehemu salama, mahali pakavu, pasafi na penye joto la wastani.
Kuku wote wanapaswa kuanza kuetamia kwa siku moja. Ili kufanikisha hili inapasa uwe karibu na kuku wako. Kuku mmoja akianza kuetamia mwekee mayai ya kuku wa kisasa au mayai mabovu ya kuku wa kienyeji. Utafanya hivi hadi kuku wako wote watakapoanza kuetamia mayai. Kuweka mayai mabovu au mayai ya kuku yaliyotumika humfanya kuku aendelee kuetamia akijua ni mayai yake.
Baada ya kuona kwamba kuku wako wote wapo tayari kwa kuetamia mayai, waandalie banda maalumu kwajili ya kuetamia yani chumba kimoja katika lile banda letu. Ninashauri kwamba chumba kwajili ya kuetamia kiwe chumba cha kwanza au cha mwisho katika mfuatano wa vyumba vya banda lako. Andaa viota bora vya kuetamia, weka mayai 20 kwa kila kiota, ikiwa hayajatimia unaweza kununua kwa wafugaji wengine ili kuifikia idadi yako.
Waamishe kuku kutoka wanapotagia na kuwaweka katika chumba ulichokiandaa kwajili ya kuetamia. Ili ufanikiwe katika zoezi hili inafaa lifanyike wakati wa usiku na unafanya katika giza. Mweke kuku katika kila kiota na asubuhi wajikute kila mmoja katika kiota chake. Wahudumie kwa chakula na maji ya kutosha. Wakati wa usiku waongezee joto la ziada kwa kuweka jiko au ndoo ya chuma yenye chengachenga za mkaa au kama una umeme weka taa za joto.
Baada ya siku 21-25 kuku wako wataanza kuangua vifaranga. Huu ndio wakati unaotakiwa kuwa karibu sana na kuku wako kuliko wakati wote. Watenge vifaranga mara tu baada ya kuanguliwa; waweke katika chumba chao maalumu mbali na kuku. Kama chumba cha kuetamia kilikuwa cha kwanza basi vifaranga wawe chumba cha mwisho n.k
Ukishawatenga vifaranga mbali na matetea wako, wawekee tena mayai mengine 20 kila tetea, mayai ambayo utayanunua kwa wafigaji wenzako. Hakikisha kuku waliotaga hayo mayai ni wazuri, hawana magonjwa na wanauzito/ukubwa unaofaa. Mayai yote yakaguliwe vizuri ili kujua kwamba yameharibika, yana nyufa au mabovu. Kabla ya kuweka mayai mengine hakikisha chumba chako ni kisafi na viota vimesafishwa, havina wadudu na uchafu wowote. Kuku wako bila kujijua wataanza kuetamia upya mayai uliowawekea.
Ukiwawekea mayai rudia mzunguko kama nilivyokwambia awali. Baada ya siku 21 hadi 25 tena utapata vifaranga wako wengine tena. Fuata kila hatua kama nilivyokwambia hapo awali. Lakini kwa awamu hii nashauri waache matetea wako wapumzike wala usiwapatie mayai mengine tena
SOURCE: KUKU PROJECT
No comments:
Post a Comment