• JIFUNZE KILIMO BORA CHA VITUNGUU

    Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu
    Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania. Afrika Mashariki, na Dunia Nzima.
    Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa mijini. Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika kutengeneza supu n.k

    Aina Za kilimo Cha Vitunguu
    Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbili
    i)    Green House
    ii)    Shambani

    Kilimo cha kitunguu Green House




    Kilimo cha vitunguu katika shamba la kawaida



    Mahitaji muhimu katika kuzalisha zao la vitunguu
    Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu
    Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu

    Kutayarisha shamba
    Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
    vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
    umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au
    majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa

    Upandaji wa mbegu za vitunguu
    Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10
    Matunzo ya bustani ya vitunguu
    Umwagiliaji

    Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba. Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua.
    Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu. Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung'olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.
    Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu
    juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongo kama sentimita 5. Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana

    Hali ya hewa na maji
    Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu.
    Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa
    wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa
    vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati wa kukomaa na kuvuna vitunguu

    Aina za vitunguu
    Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta. ikiwa kilimo bora kitazingatiwa.

    Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia
    i)    Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
    ii)    Msimu wa kupanda
    iii)    Uwezo wa kuzaa mazao mengi
    iv)    Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu

    Mbegu bora
    Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo
    i)    Uotaji zaidi ya 80%
    ii)    Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
    iii)    Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unyevu

    Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo

    i)    Chanzo cha mbegu
    ii)    Tarehe ya uzalishaji
    iii)    Tarehe ya kuisha muda wa
    iv)    Kifungashio cha mbegu.
    Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja

    Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama
    i)    ALPHA Seed Co, Popvriend,
    ii)    Rotian Seed,
    iii)    Kibo Seed,
    iv)    East African Seed Company nk

    Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya pembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.
    Nikutakie siku njema na kilimo bora, katika makala ijayo tutaangalia magonjwa yanashambulia vitunguu na jinsi ya kuweza kuyazuia.
    Makala hii imeandikwa na dirayamafanikio.blogspot.com

    No comments:

    Post a Comment