KILIMO BORA CHA ZAO LA UFUTA
MATUMIZI YA MBOLEA
Ufuta ni zao ambalo halihitaji matumizi makubwa ya Mbolea.Japokuwa hustawi zaidi katika udongo wenye rutuba ya kutosha.Kama utapanda katika ardhi isiyo na rutuba ya kutosha basi unaweza kutumia mbolea kiasi kidogo Mbolea kama vile UREA na BUSTA.
MATUNZO NA PALIZI
Miche ya ufuta ni midogo na laini sana hivyo inahitaji palizi mapema hasa katika kipindi cha majuma manne ya kwanza .Pia katika kipindi hiki unatakiwa kupunguza miche iliyosongamana.Kadri utavyochelewesha palizi na kupunguzia mimea mapema ndivyo unavyoifanya mimea isikuwe vizuri na kujipunguzia kipato chako.
MAGONJWA YA UFUTA
Magonjwa makuu ya ufuta ni madoa ya majani na kuoza matawi na shina.Zuia magonjwa haya kwa Kupanda mbegu bora na kwa kutokupanda ufuta katika ardhi inayotuamisha maji,pia itawezekana kubadilisha shamba usilime ufuta katika shamba lililolimwa msimu uliopita.
WADUDU WANAOSHAMBULIA UFUTA
Kuna wadudu wengi wanaoshambulia ufuta kama vile vibaruti (Ambao hushambulia hatua ya mwanzo kabisa ya miche iliyoota ya ufuta ambapo vibaruti hula majani ya mwanzo ya mmea mara tu yanapojitokeza).Pia Aphidi hushambulia ufuta kwa kufyonza maji katika majani ya mimea hivyo kupelekea kukauka kwa majani ya mmea.
Pia wapo funza wa majani ambao hula majani ya mimea na pia hufunga majani ya ncha ya mimea na kuzuia ukuaji wa matawi wa mimea,wadudu hawa ni hatari zaidi kwani wanazuia kutengenezwa kwa vitumba vya ufuta.
Kuzuia vibaruti,kabla hujapanda mbegu yako changanya na dawa ya tunza au gaucho.Pia panda mbegu bora na fanya mzunguko mazao shambani.Wadudu wengine wakijitokeza tumia dawa kama karate,dimethoate.Twigathoate,duduall,duduba na dawa nyingine za wadudu kabla wadudu hawajasababisha madhara makubwa shambani.
UVUNAJI
Ufuta uliokomaa tayari kwa kuvunwa utaonesha mabadiliko ya majani yake na shina na matawi yatabadilika rangi yake na kuwa njano au kahawia au yataanza kukauka,pia vitumba vya mwanzo vitaanza kubadilika rangi yake na kuanza kukauka hivyo utatakiwa ukate ufuta mapema kabla vitumba havijakauka na kupasuka.Vuna ufuta wako kwa kukata matawi ya ufuta na kuyafunga katika matita ya saizi inayokufaa ila yasiwe matita makubwa sana ambayo hayatakauka katikati kwa urahisi yasimamishe matita yako kuelekeza juu kisha acha yakauke kwa wiki mbili hadi nne kutegemea na ukali wa jua.vitumba vikisha kauka na kupasuka tandika mkeka au turubai na yageuze matita yako katika mkeka na turubai hapo ufuta utamwagikia katika mkeka au turubai lako,kuupata ufuta unaokwama katika matita piga piga kidogo tita unapoligeuza.Kisha Peta ufuta wako na kuuweka katika Vyombo safi vya kuhifadhia
SOURCE: kilimofaida
No comments:
Post a Comment