JINSI YA KUANDAA HYDROPONICS FODDER KWA AJILI YA MIFUGO YAKO 
Leo tunazidi kukuwezesha kutambua fursa lukuki ambazo zinazoweza 
kufanywa na  yeyote  katika jamii yetu.Leo tutaangalia juu ya 
hydroponic. Katika kuangalia  tutagusia vipengele vifuatavyo:
•    Utangulizi,
•    Faida ya matumizi ya hydroponic,
•    Jinsi ya kuandaa,
•    Umwagiliaji,
•    Uvunaji,
•    Mfano halisi,
•    Upatikanaji wa chakula kwa muda wote,
•    Hitimisho. 
  
UTANGULIZI
HYDROPONIC ni sayansi/sanaa ya kuotesha mazao bora yenye tija kwa muda 
mfupi zaidi bila kutumia udongo kabisa, kwa kutumia maji na virutubisho 
(Hydroponic Nutrients).
HYDROPONIC HYDROPONICS FODDER – ni kimea kinachooteshwa kwa kutumia 
mbegu za shayiri  au ngano ili kupata chakula cha mifugo mfano kuku, 
ng’ombe, sungura, nguruwe, mbuzi, kondoo n.k
Ili kuotesha mbegu zako kwa utaratibu huu utahitaji kuwa na banda maalum
 kwa kuoteshea lenye ukubwa wowote, trei za plastic au aluminium zenye 
matundu (kama ni aluminium hakikisha sio material yale yanayopata kutu 
pindi yakiingia maji).
Pia utahitaji kuwa na virutubisho vya hydroponics (Hydroponics 
Nutrients), Sprayer (Chupa ya kunyunyiza maji yenye matundu madogo ili 
maji yamwagike kama mvua), Mbegu za shayiri au ngano (chagua mbegu 
ambazo hazijashambuliwa na wadudu), na pia unatakiwa uwe na chombo cha 
kuloweka mbegu na hapa waweza kutumia ndoo ya aina yoyote, kwani 
itatakiwa uziloweke kwa siku chache.
Sayansi hii ya uoteshaji wa mbegu mbalimbali madhumuni makubwa sana ni 
kwaajili ya  mifugo kama vile, Kuku, Mbuzi, Ng’ombe, kondoo na kazalika,
 ila kama ni mboga inaweza itwa hydrponic tomatoes na kazalika kulingana
 na aina ya mbegu husika.
FAIDA YA MATUMIZI YA HYDROPONIC
Ili kuweza kukupatia picha halisi tunakufahamisha kwanza faida zilizopo 
za matumizi ya hydroponic fodder kwa mifugo.Kwa uchache baadhi ya faida 
hizo ni:
•    Ni nafuu sana kulinganisha na garama za CHAKULA cha madukani au viwandani.
•    Kina virutubisho na vitamini mara 3 zaidi ya CHAKULA cha kawaida cha Mifugo.
•    Hupunguza magonjwa ya mfumo wa hewa kama vile mafua kwa mfugaji na Mifugo kwani hakina vumbi kabisa.
•    Kina protein na Energy/nishati nyingi zaidi mara 3 ya inayopatikana kwenye vyakula vya kawaida vya Mifugo kama kuku.
•    Mifugo hukua haraka sana kutokana na wingi wa protein ambayo hufanya Kazi ya kujenga mwili na kukuza.
•    Chakula hiki ni laini sana na kitamu kwa kuku na mifugo yote (palatable).
•    Mmeng’enyo wa chakula hiki huongezeka kutoka 30% kwa chakula cha 
kawaida hadi 95% kwa chakula cha hydroponiki hivyo chakula kingi 
kutumiwa na mwili wa mifugo na kupunguza kinyesi na usumbufu wa 
usafishaji wa banda.
•    Kinyesi hupungua na kuwa kati ya 5%-10% tu kwani chakula kingi humeng’enywa na kutumiwa na mwili wa mifugo.
•    Mazao kama mayai au maziwa huongezeka kwa 40% kulinganisha na chakula cha kawaida.
•    Kiini cha yai la kuku anayelishwa hydroponic fodder huwa cha njano sana hata kama ni kuku wa kisasa.
•    Hupunguza garama za ufugaji kwenye manunuzi ya chakula kwa 50-75% hivyo kuongeza faida.
Pamoja na mnyumbulisho wa baadhi za faida ya matumizi ya teknolojia hii 
hapo juu,kiujumla ni rahisi kutumia teknolojia hii kwani inaweza 
kufanyika mahali popote. Husaidia kuvuna na kupata  mazao mengi kwa muda
 mfupi. Haina madhara kwa afya za mifugo na binadamu kama mlimaji 
alizingatia  maelekezo.
JINSI YA KUANDAA
Tumefanya tafiti kufahamu hatua kadhaa zinazopitiwa ili kufanikisha 
zoezi la upandaji.Zifuatazo ni baadhi ya hatua ambazo tumefanikiwa 
kukutana nazo:
•    Chukua mbegu zako kisha zisafishe vizuri kuondoa takataka zote.
•    Weka maji kwenye ndoo safi na kisha weka mbegu zako ili kuziloweka 
kwa muda wa masaa 4 au zaidi ukipenda masaa 12.Muda mrefu zaidi 
huwezesha mbegu kuchipua vizuri na kwa haraka.
•    Baada ya masaa 4 au 12 kupita toa mbegu zako kwenye ndoo na uzichuje maji kwa kutumia chujio au kitambaa kisafi.
•    Baada ya kuchuja maji hamishia mbegu zako kwenye tray kisha 
zisambaze ili zisibanane kupita kiasi. Kwa kuanzia fursa hii unaweza 
kutumia tray yeyote hata ungo unafaa kwa kuanzia .
•    Baada ya kuweka mbegu zako kwenye tray funika tray yako kwa muda wa
 masaa 48 (SIKU 2) tumia mfuniko wenye matundu madogo madogo na 
machache.
•    Baada ya masaa 48 kupita (siku 2) mbegu zako zitakuwa zimechipua kikamilifu, utaona mfano wa nyuzi nyeupe zinachomozo.
•    Hamishia tray zako kwenye kichanja au eneo lenye hewa ya kutosha 
lakini zikinge dhidi ya jua kali kwa kuweka turubai au nailoni juu ya 
kichanja unaweza pia kutumia hata mifuko ya unga (viloba) kutengeneza 
kichanja, unaweza pia kuzungusha wavu kama net za mbu ili kuzuia wadudu 
i.e inzi na pia kama eneo lako lina ndege wengi basi kutumia net itakuwa
 msaada kwako ili kuwazuia ndege hao.
UMWAGILIAJI
Mwagilia angalau mara 3 kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni. Hakuna
 haja ya kumwagilia usiku kwa sababu hewa ya usiku huwa imepoa na kubeba
 unyevu wa kutosha na hata asubuhi usishangae kukuta umande kwenye 
fodder yako.
UVUNAJI
Unaweza kuvuna fodder yako ndani ya siku 7 au 9.Ingawa wapo wengi 
wanavuna haraka yamkini ili kukidhi uhitaji kwa wakati husika.Lakini 
makala nyingi zinaelekeza siku 7 au 9.
MFANO HALISI
Kawaida teknolojia hii kwa mfano ukitumia kilo moja ya mbegu za ngano 
unaweza kupata mpaka kilo 8 za chakula cha kuku.Kwahiyo kwa wafugaji wa 
kuku na mifugo mingine hii ni fursa nzuri ya kupunguza gharama za 
malisho ya mifugo hii.
Ni vyema kufahamu kuwa katika kilo moja ya ngano utakuwa umeokoa 
manunuzi mengine ya kilo saba kwa kutumia teknolojia hii basi jamii 
ikitambua fursa hii itawasaidia sana katika malisho ya mifugo yao.
UPATIKANAJI WA CHAKULA KWA MUDA WOTE
Ili uweze kuhakikisha chakula cha njia hii kinakuwa tayari kwa malisho 
ya kuku wako kila siku lazima ujue mahitaji halisi ya chakula kwa siku 
moja.
Kwa mfano kama kuku wako wanatumia kilo 50 kwa siku. Kutokana na matokeo
 ya tafiti kwamba kilo 1 za mbegu zinazalisha kilo 8 za fodder kwa siku 
8, je unahitaji mbegu kiasi gani kutengeneza fodder ya kuwatosha kuku 
wako wote 350 kwa siku?.Sasa kilo 50 gawanya kwa kilo 8 za fodder 
uliyoipata kutokana na kilo 1 za mbegu, jibu lake litakuwa ni 6.25 .Hizi
 kilo 6.25 ni sawa na kilo za mbegu nitakazotakiwa kuotesha kila siku 
ili kukidhi haja ya ufugaji wako.
Kwa maana hiyo itakulazimu kupanda kilo 6.25 za mbegu kila siku katika 
tray kubwa zenye uwezo wa kubeba kilo 6.25 za mbegu. Kama utatumia tray 
moja kubwa kupanda mbegu zote hizo itakulazimu uwe na tray 8 za namna 
hiyo kwa sababu utakuwa unapanda mbegu kwenye tray kwa kupishanisha siku
 moja moja kwa maisha yote ya ufugaji na kila tray inapovunwa 
inasafishwa na kupandwa mbegu zingine siku hiyo hiyo.
HITIMISHO
Wataalamu wengi wanashauri kuwa iwapo utaamua kutumia njia hii kama 
chakula cha kuku ni vizuri pia kuwapa kuku punje kavu au mapumba matupu 
kwa uwiano wa 2 kwa 10 ili kuhakikishwa kwamba mmengenyo wa chakula 
unafanyika vizuri pasipo kuleta hatari ya constipation na siyo lazima 
kufanya hivyo kila siku. Virutubisho vilivyo kwenye fodder ya ngano au 
fodder ya shairi ni vya kutosha kabisa kwa mahitaji ya kuku wako.
Lakini  tunakiri kuwa fursa hii sio kwa wafugaji tu,bali wajasiriamali 
wanaweza kuiangalia fursa hii kwa mapana zaidi ili kuona namna gani 
wanaweza kuwekeza na kuanza kuuza kwa wafugaji wa fursa hii.
Ni fursa ambayo imeanza kufatiliwa kwa wingi kwa sasa.Nasi tunaimani 
makala hii itakuwa imekupa mwanga zaidi kwa ajili ya kuifatilia kwa 
mapana fursa hii.
Tunazidi kuwashauri kuzidi kufatilia zaidi fursa hii kwa wataalamu wa 
kilimo wa serikali na taasisi au makampuni ya kilimo yanayotambulika ili
 kuweza kupata ushauri zaidi kwa ajili ya kilimo chenye tija kwa mipango
 midogo na mikubwa.
Imeandaliwa na Edlork Team,
       

Enter your comment...nawezaje kupata hydroponics nutrients mimi niko dar es salaam, kimara
ReplyDeleteAhsante sana kwa somo,hiyo Hydroponics nutrints upatikanaji wake ukoje maana uliyopo mikoani ni shida
ReplyDelete